NGUVU YA DHAIFU SEHEMU 1&2 RIWAYA YA KUSISIMUA, NISIMULIZI YA KWELI SIKUJUWA ISOME HAPO

MNDEME BLOG
Mamaaa”
Aliniita Kareen kwa sauti ya kustua sana. Ndani ya sekunde chache akili iliwaza mambo kama kumi hivi kwa hofu. Geofrey mume wangu akanitazama, “Usiwe unastuka sana, kelele kwa watoto ni kawaida.”
Nilimpuuza na kuinuka mbio kuelekea kule nje walikokuwa wanacheza watoto. Ni kawaida kwa mtoto kuita hivyo, lakini sijui kwanini siku hiyo nilistuka sana. Ni kama nafsi yangu ilijua kuna kitu kimetokea. Ni kweli kuna kitu kilikua kimetokea, tena kitu kikubwa haswaa.

Baada ya ndoa sikupata mtoto mara moja. Niliolewa umri ukiwa umeenda kidogo tofauti labda na rafiki zangu wengi au ndugu zangu wengine.

Ingawa mimi sikuona kama ni jambo baya au huenda sikujiona nimechelewa sana, ila kutokana na walionizunguka nilihisi nitatakiwa kupata mtoto mara tu nitakapoingia kwenye ndoa. Unajua mara nyingi matatizo tunayokuwa nayo katika maisha huwa hasa matatizo kwa ajili ya jamii inayotuzunguka.

Yaani mfano mtu anayemaliza shule akakutana na changamoto ya kupata kazi, wanaomzunguka humfanya aione ni changamoto ngumu zaidi, hasa kwa maswali ya hapa na pale, mara, “Siku hizi uko wapi? Hivi kazi ulishapata? Kazi unafanyia wapi?” na maswali ya namna hiyo bila kujua kuwa unayemuuliza ana kazi au la, au ameshafanya jitihada gani za kutafuta kazi bila mafanikio.

Au yale maswali ya una watoto wangapi? Au, bado hujazaa tu? Kwa mtu aliye kwenye ndoa, bila kujali ni kiasi gani anahitaji kupata mtoto.

Mimi nakumbuka kuna mtu, tena rafiki yangu, aliwahi kuniuliza, “unakawia hivyo kuolewa, unataka uje kuzaa mjukuu? Yaani nilishindwa kumuelewa, ni kwamba mimi najioa mwenyewe au ninakataa wachumba! Mwingine nikiwa na mwaka tu kwenye ndoa aliwahi kuniambia kuwa kama nashindwa kupata ujauzito nimwambie anisaidie, pengine mume wangu ana tatizo. Huyo aliyesema hivyo ni mwanaume, na alizungumza akimaanisha kwamba anisaidie kunipa ujauzito.

Sijui kama unaelewa ukiingia kwenye ndoa na presha ya kupata mtoto haraka, miaka mitatu bila mtoto wala mimba inakua mingi kiasi gani. Yaani kuna wakati mpaka nilikuwa nahisi hata nikitembea barabarani kila mtu anajua mimi ni tasa na hivyo naona aibu. Namshukuru sana Mungu mume wangu hakuwahi kuniumiza wakati huo. Wanasema ndoa huwa zina changamoto ya mapenzi lakini mimi hilo sikuwahi kujua. 

==>Endelea
Nilipofika nje kule walikokuwa wakicheza watoto, nilikuta Karitta ameanguka chini na mate yanamtoka, mwili umekakamaa.

 Mimi nilitangulia kufika halafu Geofrey akawa nyuma yangu. Ile kelele niliyopiga, sidhani kama kuna ya namna hiyo Geof aliwahi kusikia kabla. Niliita kwa nguvu sana, Yesuuuu. Kichwani niliwaza ni kifafa, lakini mtoto alionekana kama tayari amekufa. Namshukuru Mungu nina mume asiyepaniki kama mimi.

Tulipakia mtoto kwenye gari na kwenda hospitali haraka sana. Kareen alimshika dada yake huku akilia tu tukiwa kwenye gari, akijitahidi kumuamsha. Nilihisi tumbo la kuhara limenishika, halafu likawa linakata tena kama tumbo la uzazi. Akili ilizunguka kwa mawazo. Nilijaribu kuomba ila maombi yaligoma kabisa.

Unajua ni vyema kuwa mtu wa maombi wakati hali ikiwa shwari kabisa, kwani linapotokea janga, hujui kama utapata hizo nguvu za kusali. Geof aliendesha gari huku akikemea na kuomba kwa sauti. Nikawa tu nikiitikia amen lakini akilini hata sijielewi.

Tulifika hospitali moja, sitaitaja jina, wakampeleka chumba cha wagonjwa wa dharura yaani emergency na kuanza kumshughulikia.

Walipima vipimo vya awali na kusema hawaoni kitu, wakawa wanamuhudumia tu kwa dripu na mashine za kupima mapigo ya moyo. Kesho yake kuna daktari alikuja na kumpima vipimo vingine pia akasema haoni tatizo, akadai inawezekana ni kifafa tu, wakati huo mwanangu hajitambui na hali iko vilevile. Sikuwa na uzoefu sana kuhusu kifafa lakini kwa uelewa wangu nilihisi ingekuwa kifafa basi angeshapata fahamu.

Nilikasirika, tukalazimisha siku iliyofuata tumtoe mtoto, tukamuhamishia hospitali nyingine. Walipopima waliona malaria iliyoingia kwenye ubongo. Kwa watoto wa umri chini ya miaka mitano malaria ni hatari sana, na hii nadhani wazazi ni muhimu kutilia mkazo zaidi. Tatizo pia kuna wakati hospitali vipimo vya malaria vinaonyesha hasi (negative) hata wakati ipo (positive). 


Comments

Popular posts from this blog